DKT. MSONDE AMTEMBELEA RAS DODOMA KWA MAZUNGUMZO
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde, leo Februari 24, 2025, amemtembelea Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya Ofisini kwake Jengo la Mkapa Jijini Dodoma kwa lengo la kuzungumza juu ya mabadiliko ya mfumo wa malipo kwa huduma kutoka kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania, TEMESA.
Dkt. Msonde amemueleza Katibu Tawala Mkoa kwamba, Wakala huyo anapitia changamoto mbalimbali zinazosababisha kulemewa na mzigo wa madeni kutokana na huduma wanazozitoa kushindwa kulipiwa kwa wakati hasa utengenezaji wa magari ya Serikali.
“Tumekuja na mapendekezo kwa Serikali ambayo yamepitishwa na Mhe. Rais kwamba kuanzia Januari, 2025, Mfumo wa malipo ya huduma kwa TEMESA yatakua kwa ‘pre-paid’, kama utapeleka gari pale basi ulipie kabla au baada ya matengenezo kwa control namba na lengo ni kufikia Julai mosi 2025, mwaka mpya wa fedha, hatutaki kusikia TEMESA inadaiwa” Dkt. Msonde.
Aidha, Bw. Mmuya amempongeza Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kuja na mfumo huo kwani utakua muarobaini wa mzigo wa madeni kwa Wakala huyo.
“Ulichokisema nimekifurahia kwani umekwenda kutafuta mzizi wa tatizo kwani hapa hatutafuti thamani ya pesa bali usalama wa magari na viongozi wetu. Watumishi wetu wote wakienda kwenye hilo, tutafika mbali. Uwekezaji huu ukileta manufaa makubwa, hata viongozi wetu wanaokuja watasema huu ndio mwokozi wetu”.
Katika mzungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu aliambatana na viongozi wa Wizara yake, Wakala wa Majengo TBA pamoja na wale wa TEMESA huku wa Mkoa wakiwa ni Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment