MAKALA FUPI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Na: Hellen M. Minja,
Habari - DODOMA RS
Maadhimisho ya kilele cha siku ya Wanawake Duniani, hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 08. Kuelekea maadhimisho hayo Kitaifa 2025, yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Arusha, huku Mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan,
Mikoa ya Dodoma,Singida na Iringa imeandaa Kongamano kubwa litakalowakutanisha Wanawake wa mikoa hiyo, Mkoa wa Dodoma ukiwa mwenyeji wa Kongamano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma Machi 03, 2025.
Lengo la Kongamano hilo ni kumtambua Mwanamke katika nafasi ya Uongozi,ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Anna Makinda. Ni hatua muhimu katika mfumo wa maisha ya mwanadamu inayolenga kuhakikisha kuwa na fursa sawa kwa wote na kushiriki kwenye Uongozi na maamuzi yote katika jamii.
Kongamano hilo pia litasadifu lengo la maadhimisho ya siku ya Mwanamke Duniani ambalo ni kuongeza idadi ya Wanawake ili kuwa na uwakilishi wa kutosha kwenye nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya msingi,kati hadi juu, kwa wanawake wenye taaluma, utakaosaidia kuwa na mipango inayozingatia mahitaji ya kijinsia kwa makundi yote ya kijamii.
Mpango huu ni pamoja na kupigania kuwepo kwa sera, miongozo, sheria na kanuni ambazo zinalinda haki ya kijinsia na usawa kwenye Uongozi. Wanawake watajengewa ujuzi, taaluma na uwezo wa kujiamini, kujitambua, uthubutu wa kufanya maamuzi na kutenda kwa ajili ya maslahi ya Umma.
Matukio yatakayoambata na Kongamano hilo litakaloanza saa 2:30 asubuhi, ni pamoja na utoaji wa tuzo/vyeti kwa wananwake vinara waliojitoa na kuwezesha usawa wa kijinsia kwenye jamii, utoaji wa huduma za afya kwa wananchi watakaoshiriki siku ya kilele, uchangiaji wa damu, upimaji wa Saratani ya shingo ya kizazi, Saratani ya matiti, upimaji wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, maonesho ya nishati safi ya mkaa ya vikundi vya wanawake, maonesho ya bidhaa za wanawake wajasiriamali pamoja na kusikiliza shuhuda mbalimbali kutoka kwa Wanawake waliofanikiwa wa Mikoa ya Singida, Iringa na Dodoma.
Siku ya Wanawake Duniani 2025 ambayo Kitaifa hufanyika kila baada ya miaka mitano(5), inakwenda sambamba na kaulimbiu ya “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” ambapo matarajio ya Kongamano hilo ni kuwapa mwanga Wanawake ili waweze kujiamini na kupata uzoefu kutoka kwa wanawake vinara kujua mbinu walizopitia hadi kufikia hapo walipo. Wanawake wote wa Dodoma na mikoa jirani wanakaribishwa kushiriki Kongamano hilo.
Comments
Post a Comment