MAKAMU WA RAIS AIFARIJI FAMILIA YA MAREHEMU NKONDO

 












Na Sofia Remmi.
Habari-Dodoma Rs

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wameifariji familia na waombolezaji mbalimbali kufuatia kifo cha Bw. Johnson Nkondo aliyekuwa Msaidizi wa Ofisi Mkuu - Ofisi ya Makamu wa Rais aliyefariki tarehe 13 Februari 2025 katika Hospitali ya Benjamini Mkapa mkoani Dodoma wakati akipatiwa matibabu.
 
Makamu wa Rais na Mwenza wake wametoa faraja hiyo walipowasili katika makazi ya familia ya Marehemu Johnson Nkondo eneo la Veyula Mkoani Dodoma leo tarehe 16 Februari 2025.
 
Akizungumza na waombolezaji, Makamu wa Rais amesema marehemu Nkondo alikuwa muadilifu aliyezingatia maadili ya Utumishi wa Umma na taratibu za kiofisi wakati wote wa utumishi wake. Amesema ni vema kumuenzi marehemu Nkondo kwa kujifunza namna alivyojitolea kulitumikia Taifa kwa uadilifu mkubwa pamoja na kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake vema, kuishi vema na ndugu, majirani na marafiki.
 
Makamu wa Rais amewaombea faraja ya Mwenyezi Mungu iwafikie familia, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule aliyeshiriki katika msiba huo, ametoa pole kwa familia na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kumpoteza mtumishi hodari. Amewasihi familia na waombolezaji kuendelea kumuomba Mungu awavushe salama katika kipindi kigumu cha msiba huo.
 
Marehemu Johnson Nkondo alizaliwa tarehe 20 Aprili 1966 na anatarajiwa kuzikwa tarehe 17 Februari 2025 kijijini kwao Bombo Wilaya Same mkoani Kilimanjaro.










Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA