VIJANA WAASWA KUTOJIINGIZA KWENYE MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA
Na Sofia Remmi.
Habari-Dodoma Rs
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mheshimiwa Rosemary Senyamule amewataka Vijana kuacha kujaribu kila kitu,kwani kwa kufanya hivyo,baadhi yao wamejikuta wakijiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ambayo matokeo yake ni kumomonyoka kwa maadili na kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo Machi 28,2025 wakati wa Kongamano la Vijana la Kupinga Matumizi ya Dawa za kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Tasisi isiyo ya kiserikali ya Taifa Forum.
"Sumu haionjwi,Wazee sio wepesi kujaribu kila kitu.Lakini Vijana mmekuwa wepesi kujaribu kila kitu, katika kujaribu huko, mnajikuta mmeingia kwenye kutumia Dawa za kulevya,kitu ambacho kinaharibu maisha yenu,kinasababisha mmonyoko wa maadili,lakini pia kinapunguza nguvu kazi ya Taifa.Acheni kujaribu kila kitu, ukiambiwa kitu hiki hakifai,acha,usijaribu kukifanya".Amesema Mhe. Senyamule
Mhe. Senyamule ameongeza kuwa nguvu kazi imekuwa ikipotea na chanzo cha yote ni Vijana kujiingiza kwenye dawa za kulevya,hivyo inawapasa kuepuka kutokujiingiza huko.
Aidha, amewataka Vijana kutumia Mitandao ya Kijamii kwa faida badala ya kukesha kwenye mitandao kwa kuandika na kusoma vitu vinavyopotosha maadili.
Kadhalika, Mhe. Senyamule amewataka vijana kuwa makini na kuacha kudanganywa katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani na ikibidi nao wajitokeze kugombea.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi, sisi Tanzania tunahitaji amani, tunahitaji utulivu na watu wetu wanahitaji kuona tukiendelea kuwa hivyo, naomba mjiepushe na hayo yote lakini kikubwa tumieni TEHAMA kwa kuwa na tija,” amesisitiza Mhe.Senyamule.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya 'Taifa Forum' Charles Hadson amesema kuwa kongamano hilo ni la pili kufanyika, ambapo mwaka jana aliwakutanisha vijana kwenye kongamano kubwa kama hilo Jijini Mwanza na kuwa matunda yake wameanza kuyaona.
Hadson amesema kwa Jiji la Dodoma wanaamini kuwa Vijana wa Vyuo watakwenda kuwa Mabalozi wazuri kwenye kuwaelimisha vijana wenzao ili waweze kuepukana na mtindo wa kuiga maisha.
Kwa upande wake Afisa wa Kudhibiti dawa za kulevya Kanda ya Kati Anna Tengia amesema kuwa katika Mikoa ya Kanda ya Kati Vijana wanaumizwa zaidi na dawa ya kulevya aina ya Scanka ambayo inaharibu ubongo wao, hatimaye inawafanya kushindwa kufikiri vizuri.
Anna ametaja umri ambao unapata tatizo hilo ni kuanzia miaka 13 hadi miaka 35 hivyo ameomba Wazazi kuwa makini zaidi na watoto wao ili kuwasaidia kuvuka katika umri wenye ushawishi na kufikia umri wa kutambua mema na mabaya.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali ikiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa,Vijana kutoka vyuo mbalimbali vya Jijini Dodoma wameshiriki.Huku Vijana waliokuwa warahibu wa dawa hizo ambao wameamua kuacha wakitoa shuhuda zao juu ya namna walivyoingia katika janga hilo,na athari walizozipata.
Comments
Post a Comment