VISIMA 7 VYA UMWAGILIAJI KULETA MAPINDUZI MAKUBWA KWENYE KILIMO DODOMA
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kufanya Mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo Mkoa wa Dodoma kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambapo Machi 28,2025 Tume hiyo imefanya uzinduzi wa Mradi wa uchimbaji wa visima 7 vya umwagiliaji katika Kata ya Matumbulu Jijini humu.
Akizindua mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa Mapinduzi haya yanahitaji ushirikiano wa pande zote mbili ili kuleta matokeo chanja katika Kilimo.
“Haya ni Mapinduzi lakini yanataka pande zote, upande huu wa Serikali Mhe. Rais anakua amemaliza kwa kujenga kisima, upande wenu ni kuhakikisha taratibu zote za kutumia hii rasilimali, kisima hiki kilete tija inayokusudiwa na Serikali na faida kwa maisha yenu kama matamanio ya Serikali yalivyo.”
Akizungumza na Wananchi hao, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mhe. Anthony Mavunde, amesema kazi ya uchimbaji wa kisima inayofanyika hapo inakwenda kuongeza wigo mpana kwa Wakulima kulima kwa tija kwani changamoto kubwa hasa kwenye zao la Zabibu ni kilimo cha tija ambacho kitamfanya mkulima alime eneo dogo apate mazao mengi.
Kadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mlolwa amesema Tume ina mpango wa kujenga njia za umwagiliaji kwenye mashamba hivyo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Kata ya Matumbulu, watafanya usanifu wa eneo na kuweka kwenye ramani moja ili kupata idadi ya mabomba pamoja na aina ya tenki la kuhifadhia maji litakalojengwa katika eneo hilo.
Mradi wa uchimbaji wa visima ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais kwa Tume hiyo kuwawezesha Wakulima wadogo kwa kuwawekea miundombinu ya umwagiliaji ili waweze kulima angalau heka 1 au 1 na nusu ambapo mradi huo utatekeleza uchimbaji wa visima zaidi ya 68,000 Nchi nzima ambapo kwa Mkoa wa Dodoma, unatekeleza uchimbaji wa visima 7 vya umwagiliaji.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment