KILELE CHA MAADHIMISHO YA MUUNGANO WA TANZANIA: MSISITIZO WATOLEWA JUU YA ULINZI WA MUUNGANO
Na. Hellen M. Minja,
Habari - DODOMA RS
Ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 2025 ambayo yamekwenda sanjari na hitimisho la ziara ya siku nne (4) ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Stephen Wasira katika Mkoa wa Dodoma, ametembelea miradi kadhaa ya maendeleo katika Halmashauri za Chemba, Kondoa na Kondoa Mji sambamba na kuongea na wananchi kwenye Halmashauri hizo.
Katika kilele cha Maadhimisho hayo, Ndugu Wasira ameendelea kusisitiza juu ya kutunza Muungano wetu ambao waasisi wake Hayati Mwl. Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanganyika na Hayati Abeid Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar waliupigania na kuzaliwa nchi ya Tanzania kwa ajili ya kutunza Amani na maendeleo ya vizazi vyote.
"Kuwa na nchi mbili kama hazielewani, matatizo ya kiusalama ni makubwa sana, moja ya sababu zilizofanya tukaungana ni kuweka nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuweka amani ambayo ndio msingi wa Maendeleo yote mnayoyaona na tumeungana kwa sababu ya kuweka maendeleo ya kizazi cha wakati ule, cha sasa na vinavyokuja" Ndugu Wasira.
Aidha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Alhaji Adam Kimbisa amesema, Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta miradi mingi ya elimu, Afya na maji kwenye Halmashauri za Chemba na Kondoa ikiwa ni katika kutimiza wajibu wake kwa wananchi hao hivyo wanapaswa kuonesha shukrani zao kwake.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Fatma Nyangasa, amesema "Muungano umeendelea kuwa Tunu katika Taifa letu na katika kipindi cha miaka minne ya Mhe. Dkt. Samia, Wilaya yetu imepokea na kutumia jumla ya shilingi Bilioni 71.9 katika maeneo mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Halmashauri ya Mji Kondoa".
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Ndugu Wasira ametembelea Mradi wa Ujenzi wa shule maalumu ya wavulana ya Kanda inayojengwa Chemba kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.1, kupitia Mpango wa kuboresha Elimu Sekondari (SEQUIP) ikiwa na majengo 38 na unatarajiwa kupunguza changamoto za Elimu kwa wanafunzi 960 wa Kanda ya Kati kwa ngazi za O- level na A-level.
Akiwa Wilaya ya Kondoa, alitembelea Mradi wa Hospitali ya Wilaya ambayo ilianza mwaka 2021 kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.5 lakini mpaka Sasa Halmashauri imepokea Bilioni 3.5. Hospitali hiyo inahudumia zaidi ya watu 250,000 wa ndani na nje ya Wilaya hiyo. Mradi mwingine ambao pia uliwekwa jiwe la msingi ni Ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata ya Suruke ambao umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 544.2
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
#karibumwengewauhuru2025mkoawadodoma
#miaka61yamuunganowatanzania2025
Comments
Post a Comment