UHAKIKI ANUANI ZA MAKAZI KUANZA MEI 28 DODOMA
Na Sizah Kangalawe
Habari- DodomaRS
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu zoezi la uhakiki wa taarifa za anuani za makazi, linalotarajia kuanza Mei 28/ 2025 katika Halmashauri za Mkoa wa Dodoma.
Mmuya amesema hayo wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa hizo Mei 26/2025, Katika ukumbi wa Mikutano wa Four point Hotel Jijini Dodoma, uliowahusisha watendaji kata, wenyeviti wa Serikali za mitaa na vijiji na Maafisa Tarafa.
‘’Wakurugenzi wote, hakikisheni mnasimamia zoezi hili katika halmashauri zenu huku mkitambua kuwa ni zoezi endelevu hivyo sitegemei kusikia mmeacha kuhuisha taarifa baada ya siku za zoezi hili kumalizika.
‘’Vilevile hakikisheni mnatumia Mfumo wa anuani za makazi kutambua makazi na wakazi katika maeneo yenu ili kuongeza ufanisi katika kusimamia mazoezi mbalimbali ya kitaifa na kupanga mipango ya maendeleo’’, Amesema Mmuya
Akitoa salamu za Jiji la Dodoma Meya wa jiji hilo Prof. Davis Mwamfupe amesema Jiji hilo limejitanabaisha kuwa Jiji nadhifu na litakalokuwa mfano kwa kutoa huduma bora.
‘’Uhakiki huu tunaokwenda kuufanya unakwenda sambamba na ukweli kwamba Dodoma tumejitanabaisha kwamba ni mji nadhifu , sio kwa maana ya usafi tu lakini ‘Smart City’ ambayo sasa utoaji wa huduma lazima uwe katika kiwango cha juu’’ ameweka bayana Prof. Mwamfupe
Baada ya uzinduzi wa zoezi hilo kutafanyika mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa Serikali za mitaa na kata ya kuwawezesha kufanya zoezi hilo katika ubora unaotakiwa na zoezi la uhakiki litafanyika kwa siku 12 kuanzia tarehe 28/05/2025.
Zoezi la uhakiki wa anuani za Makazi, linafanyika chini ya uratibu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wataalamu wa ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Comments
Post a Comment