WANAFUNZI WAHIMIZWA KUENDELEZA VIPAJI WALIVYONAVYO KWAKUWA NI FURSA YA AJIRA.

 




















Na; Happiness E. Chindiye 
      Habari - Dodoma RS

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule amewataka wanafunzi wa Shule za Msingi kutoka Halmashauri zote nane za Mkoani hapa ambao wapo katika kambi ya siku saba ya kuandaa timu itakayowakilisha Mkoa kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yatakayofanyika Kitaifa Mkoani Iringa kuendeleza vipaji walivyonavyo kwa kuwa ni fursa ya ajira kwa siku zijazo.

Wito huo umetolewa  Mei 27,2025 wakati akizindua rasmi mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa ambayo yanalenga kuunda timu ya Mkoa itakayowakilisha kwenye mashindano ya Kitaifa yatakayofanyika mkoani Iringa kuanzia Juni 08 mwaka huu.
 
“ Mkoa wa Dodoma tunasema ni fahari ya Watanzania, tunataka isiwe kwenye elimu peke yake tunataka iwe kwenye mchezo na sekta nyingine zote.Hakikisheni kwa hii wiki moja mnajifunza vizuri ili mkatuwakilishe Kitaifa na mshike namba moja hivyo tumieni hii wiki vizuri Mkoa unatamani kuona matokeo haya,hauendi kwa ajili yako peke yako bali ni kwa Mkoa.

“ Lakini ninyi kama wachezaji vipaji hivyo mkiviendeleza vizuri vinakuja kuwa ajira inakuwa ni faida yenu , ili iwe ajira lazima uonyeshe kipaji chako isiishie kwenye mdomo tu onyesha uwezo wako mkubwa kwa kujitofautisha na wengine “. - Mhe. Senyamule 

Kwa upande wake Afisa Michezo wa Mkoa wa Dodoma Bw. Evance Sangawe pamoja na kueleza hali ya kambi hiyo ameainisha michezo mbalimbali itakayoshindaniwa na washiriki hao.

“ Mkoa wetu wa Dodoma tuna programu ya vitalu ambapo kunakuwa na eneo maalum la kuandaa Wanafunzi kwa ajili ya mchezo ili kukuza vipaji huku mchezo ambayo tutashiriki ikiwa ni pamoja na Mpira wa mguu, Mikono, kwaya , na kadharika. ” - Bw. Sangawe 

Naye, Fatuma Jonas Mwanafunzi kutoa Shule ya Msingi Lamaiti kutoka Bahi akizungumza kwa niaba ya wenzake  ambao wanashiriki mashindano hayo kutoka katika halmashauri za mkoa wa Dodoma ameeleza namna wanavyojiandaa ili wafanye vizuri katika mashindano ya Kitaifa.

“ Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaenda kuwakilisha Mkoa wa Dodoma kwenye mashindano hayo ya UMITAMSHIMTA mkoani Iringa kwa kurudi na ushindi mkubwa kwani michezo ni mingi hivyo tuna imani tutashinda” 



#dodomafahariyawatanzania
#wekezadodomastawishadodoma
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
















Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WA HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

‘WANAWAKE NA SAMIA’ 3000 MKOA WA DODOMA KUPATA MAFUNZO VETA