SERIKALI IMEJIPANGA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA : WAZIRI GWAJIMA
Na; Happiness E. Chindiye
Habari - Dodoma RS
Serikali imejipanga vema kupambana na tatizo la dawa za kulevya kwa kuanzisha chombo mahsusi kijulikanacho kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ambacho pamoja na majukumu mengine ina jukumu la kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya, kuratibu na kusimamia masuala ya tiba na huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya Nchini ikiwemo nyumba za upataji nafuu.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Doroth Gwajima wakati la Kongamano la Vijana lililo andaliwa mahususi kwa ajili ya elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya lililofanyika ukumbi wa Mabele Jijini Dodoma.
“Mamlaka yetu ina jukumu la kutoa elimu sahihi kwa Umma juu ya athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya, kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.
“Kwa hiyo tukio letu la leo linashabihiana kabisa na malengo na mikakati ya Serikali katika kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya. “ - Mhe. Gwajima
Hata Hivyo, Mhe. Gwajima amewasihi Vijana kuwa mabalozi wazuri wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA), Bw. Aretas Lyimo amewaasa vijana kuachana na Matumizi ya dawa za kulevya kwani yanazima ndoto na kuweza kuwaingiza kwenye matokeo mabaya, ikiwa ni pamoja na uraibu, vitendo vya ukatili, matatizo ya kiafya kama vile UKIMWI, Magonjwa ya Akili, Kifua Kikuu pamoja na Homa ya Ini.
Kongamano hili ni mojawapo ya matukio yaliyopangwa kufanyika kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani ambayo yanatarajiwa kufanyika Juni 26,2025 Jijini hapa.
#drugday2025
#wekezakwenyekinganatibadhidiyadawazakulevya
Comments
Post a Comment