SHUGHULI ZA KIBINADAMU ZATAJWA KUWA TISHIO KWA CHANZO CHA MAJI BONDE LA MAKUTUPORA JIJINI DODOMA
Na. Hellen M. Minja
Habari – DODOMA RS
Uvamizi wa vyanzo vya maji kwa shughuli za kibinadamu unatajwa kuwa changamoto inayoendelea kuvikabili vyanzo vya Maji hususan kile cha Bonde la Makutupora (Kidakio cha Kinyasungwe).
Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha jukwaa la Wadau wa maji sekta Mtambuka Kidakio cha Kinyasungwe Jijini Dodoma.
Kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya, kimefanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya ‘Midland View Inn’ Kisasa Jijini hapa, kimelenga kujadili mambo kadhaa yanayokikabili Kidakio hicho ambacho ni chanzo muhimu cha maji kwa Jiji la Dodoma.
“Kuna uvamizi wa vyanzo vya maji vinavyotegemewa na Jiji la Dodoma kama vile maeneo tengefu ya hifadhi ya maji chini ya ardhi. Uvamizi huu upo maeneo mengi mno, kuna wengine wanakwenda kulima, kukata miti na shughuli nyingine. Hii changamoto ishughulikiwe, eneo lile litunzwe kwani faida yake tunayo sisi Wanadodoma”. Bw. Mmuya
Kadhalika, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandishi Elibariki Mmasy, amesema maendeleo ya Jiji la Dodoma yanategemea uwepo wa maji katika vyanzo vya Makutupora, Nzuguni na Chamwino hivyo kama Taasisi wana wajibu wa kuwakusanya Wadau na kujadili ni jinsi gani wanalinda vyanzo hivyo.
Jiji la Dodoma linaangukia ndani ya Hifadhi ya Maji ya Kinyasungwe (Makutupora) ambapo linanufaika na maji yanayopatikana katika eneo hilo kwa 100% hali inayochagiza ukuaji wa uchumi na Maendeleo ya Jiji hili hivyo ni muhimu kutunza chanzo hiki ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kwa mustakabali wa Taifa kwa ujumla.
#dodomafahariyawatanzania
#wekezadodomastawishadodoma
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment